Home | The Ministry | Service Charter | Projects | Policies | Publications | News & Events | Speeches | Tenders | FAQ | Links | Contact Us
rss
Subscribe to RSS News
Comments / Maoni

Ministry of Infrastructure Development

Its mission is to facilitate provision of an economic, safe and reliable construction industry, transport and services, meteorology, electrical and mechanical services, government buildings and stores that meet the needs of the public through development and implementation of appropriate sector policies, strategies and standards.

News and Highlights

Sheria mpya ujenzi wa majengo yaja

Serikali itafanya marekebisho na kutunga sheria mpya ya ujenzi wa majengo, Bunge limeelezwa.

Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema hayo mjini hapa jana, alipowasilisha Mpango wa Maendeleo na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2008/2009.

Alisema serikali inaendelea na ukamilishaji wa mchakato wa kurekebisha na kutunga sheria mpya ya ujenzi wa majengo.

Hatua hiyo ya serikali imefikiwa, ikiwa ni wiki chache baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 10 jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine watatu kujeruhiwa.

Dk. Kawambwa aliyeliomba Bunge kuidhinisha sh. 801,961,340,900 kwa ajili ya matumizi ya wizara, alisema Bodi ya Usajili wa Wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi, inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya kutokamilika kwa sheria ya majengo.

Alifafanua kwamba, kuwepo kwa sheria hiyo kutasaidia kuainisha viwango vya ujenzi na kuweka ubora unaotakiwa kulingana na matumizi ya jengo, hususan ya shughuli za kijamii.

"...Pia itawezesha kuanisha ujenzi sawia na mipango ya miji mbalimbali," alisema na kuongeza kwamba, wizara inaendelea na utaratibu wa kukamilisha mchakato wa kurekebisha Sheria namba 16 ya mwaka 1997 iliyounda bodi hiyo.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, Bodi hiyo inatarajia kusajili wataalamu 70 na wale wenye sifa za kati 53.

Bodi pia inatarajia kusajili kampuni za kitaalamu 53 na kutahini wataalamu 112, huku ikiendelea na mpango wa mafunzo maalumu ya vitendo, kuwasaidia wahitimu 60 wa taaluma hiyo waweze kusajiliwa.

Dk. Kawambwa alisema Wakala wa Majengo ya Serikali (WBA), umejenga maghorofa 278 katika mikoa 21 nchini, huku ofisi mpya zinazojengwa zinazingatia mahitaji ya walemavu.

Alisema wakala huo una mpango wa ujenzi wa nyumba nyingine jijini Dar es Salaam, eneo la Kigamboni, ambako kuna viwanja vyake.

Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Miundombinu, iliitaka serikali itunge sheria mahsusi ya ujenzi, kwani kukosekana kwake kunatoa mwanya kwa ujenzi holela.
Imeitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wanaokiuka sheria na taratibu za ujenzi, ambao umekuwa chanzo cha madhara mengi, yakiwamo maafa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Missanga, alisema kutokuwepo kwa sheria rasmi ya majenzi, kunachangia kuwepo kwa matukio ya ujenzi usiokuwa na viwango.
"…kamati inaitaka serikali kuharakisha kutunga sheria hiyo,” alisema Missanga, Mbunge wa Singida Kusini kupitia CCM.

Missanga pia aliitaka serikali kutoa adhabu kali kwa wahusika waliosababisha kuanguka kwa jengo la ghorofa 10 katika eneo la Kisutu, Dar es Salaam.

Hata hivyo, watuhumiwa wa tukio hilo wakiwemo mhandisi, msanifu wa jengo na mhandisi wa Manispaa ya Ilala, wamekwisha kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameunda tume maalumu kuchunguza suala hilo.

Kamati imeitaka serikali katika mchakato wa kutoa vibali vya ujenzi, kuhusisha Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC), Bodi ya Usajili wa Wasanifu na Wakadiria Majenzi (AQSRB) na wataalamu wa mipango miji.

Naye Daniel Nsanzugwanko (Kasulu Mashariki-CCM), licha ya kutaka zichukuliwe hatua kali, aliitaka Wizara ya Miundombinu kuharakisha marekebisho ya sheria.
Alisema kuna madai kuwa, ERB inazuia mapendekezo ya mabadiliko ya sheria kuhusu ujenzi.

Katika hatua iliyoonekana ni kujibu ‘vijembe’ vya kambi ya upinzani, Nsanzugwanko, alisema mikakati yote inayofanyika na miradi iliyotekelezwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Awali, akiwasilisha hoja ya kambi ya upinzani, Waziri Kivuli Kabwe Zitto (Kigoma Kaskazini-CHADEMA), alisema jimbo lake limekuwa la kwanza katika historia ya Kigoma kupata barabara ya lami.

Na Peter Orwa, Dodoma

Ministry of Infrastructure Development

Tancot House, Pamba Road / Sokoine Drive, P.O. Box 9144, Dar es Salaam | Phone +255 22213 7650 - 6 | Fax +255 222112751