
Hon Dr.Shukuru Kawambwa(MP) Minister of Infrastructure Development


Site Search
Reports & Policies
To facilitate provision of an economic, safe and reliable constriction industry, transport and services, meteorology, government buildings...

Ministry of Infrastructure Development
Its mission is to facilitate provision of an economic, safe and reliable construction industry, transport and services, meteorology, electrical and mechanical services, government buildings and stores that meet the needs of the public through development and implementation of appropriate sector policies, strategies and standards.
Speeches and StatementsHOTUBA YA RAIS: MKUTANO WA MASHAURIANO KWA MWAKA 2009 WA BODI YA USAJILI WA MAKANDARASI (CRB)MKUTANO WA MASHAURIANO - CRB 2009
Kwanza kabisa, nakushukuru wewe Waziri na Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa kunikaribisha na kunishirikisha kwenye mkutano huu muhimu. Nawashukuru kwa burudani kutoka vijana wa THT.Mwaliko wenu huu umenipa fursa ya kukutana na kuzungumza na wadau wa shughuli ya ukandarasi hapa nchini watu ambao ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu. Ndugu Mwenyekiti wa Bodi, Ndugu Msajili wa Makandarasi; Napenda kuwapongeza kwa mambo mawili. Kwanza, kwa kuwa na utaratibu huu mzuri wa mikutano ya mashauriano kati ya Bodi ya Usajili wa Makandarasi na wadau wa sekta ya ujenzi nchini. Hii inadhihirisha kwamba Bodi ipo makini, inatambua wajibu wake na iko tayari kuutekeleza. Nafurahi kwamba mwaka huu mmechagua jambo muafaka kuwa mada kuu ya mkutano wenu. Kuzungumzia suala la upatikanaji wa thamani ya fedha kuwa jambo la msingi katika kuwa na miundombinu endelevu na kupunguza umasini au kwa lugha ya kigeni (value for money in construction: a key for sustainable infrastructure delivery and poverty reduction) ni jambo la msingi. Pili, nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kusimamia ubora wa kazi za makandarasi nchini. Nimesikia maelezo ya Mwenyekiti wa Bodi pamoja na maelezo ya Msajili na nimeridhika na kufurahishwa na jitihada mnazofanya katika kusimamia, kuratibu na kuwaendeleza makandarasi kwa nia ya kuwalinda wateja wao na watumiaji wa huduma zinazotolewa na makandarasi. Aidha nafurahi kwamba kwa kufanya hivyo, mnahakikisha kuwa kazi iliyofanywa inalingana na thamani ya pesa (value for money) iliyotumika katika miradi iliyojengwa. Nimefarijika sana na hatua zinazofanywa na Bodi yenu katika kushughulikia makandarasi wasiotimiza ipasavyo wajibu wao ama kwa kukosa uwezo au kwa uzembe. Kujenga jengo linalobomoka kabla ya kwisha, au daraja linalopata nyufa miezi mitano baada ya kutumika au kujenga barabara ambayo lami huanza kubanduka kabla barabara haijesha au mradi kuchukua miaka mingi kwisha ndo vinavyoivunjia heshima shughuli ya ukandarasi na taaluma nzima ya uhandisi na usanifu. Mheshimiwa Waziri, Ndugu Washiriki; Nimetiwa moyo sana kusikia jitihada za Bodi za kuwajengea uwezo makandarasi. Nawapongeza sana kwa kubuni wazo zuri la kuanzisha Mfuko wa Makandarasi, ambao utawasaidia makandarasi wadogo kwa kuwapatia Dhamana ya Kuombea Kazi (Bid Bond) na Dhamana ya Malipo ya Awali (Advance Payment Guarantees). Pia, mmefanya uamuzi wa busara wa kuanzisha Mpango Endelevu wa Mafunzo ya Makandarasi ili kuinua uwezo wa makandarasi katika nyanja zote zinazohusiana na huduma hii muhimu. Napenda nichukue fursa hii kuwahakikishia kuwa Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Bodi ya Usajili katika kujenga msingi imara wa shughuli za ukandarasi hapa nchini. Ni matumaini yangu kuwa makandarasi mtatumia ipasavyo fursa hizi kwa manufaa yenu binafsi, kwa manufaa ya sekta na Taifa kwa ujumla. Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Washiriki; Nimeridhishwa na maelezo ya Mwenyekiti na Msajili wa Bodi, kwamba dukuduku nilizokuwa nazo kuhusu mwenendo wa huduma ya ukandarasi zinafanyiwa kazi. Kwahiyo, leo nitakuwa na machache sana ya kuzungumza. Kwanza, naomba nianze kwa kusema kwamba, kama mnavyofahamu, serikali ni mdau na mtumiaji mkubwa wa huduma za makandarasi. Sisi katika Serikali tunatambua umuhimu wa pekee wa makandarasi kwa maendeleo ya Taifa letu. Miundombinu ya aina zote, barabara, reli, viwanja vya ndege, mifumo ya maji, majengo mbalimbali ya Serikali, makampuni na watu binafsi, migodi, viwanda, minara ya mawasiliano, n.k yote hayo ni matokeo ya kazi za makandarasi. Ni dhahiri kuwa ubora na ufanisi wa kazi za makandarasi ni muhimu sana katika kujenga na kusukuma mbele maendeleo ya Taifa letu. Ndio maana nafurahishwa na jitihada zenu za kuimarisha ubora na ufanisi wa kazi za makandarasi. Katika kipindi hiki, ambapo Serikali imetenga kiasi kikubwa cha bajeti yake kwa ajili ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, maji, umeme, elimu, afya n.k. suala la ubora wa kazi za makandarasi ni muhimu sana kwetu sisi katika Serikali. Hali kadhalika mwekezaji katika sekta binafsi na miradi na watu binafsi Jitihada zote za Serikali kuwekeza kwenye miundombinu pamoja na sekta binafsi na watu binafsi haziwezi kuwa na manufaa yeyote yale kama kazi zitakayofanywa hazitafikia viwango vya ubora vinavyohitajika. Dhamana ya kuhakikisha kuwa Serikali na kila mwekezaji anapata thamani ya fedha anayotumia katika miradi ya ujenzi ni yetu sote: nyie Makandarasi na sisi tunaowapa kazi katika Serikali sekta binafsi. Ndugu Makandarasi; Ninyi mnayo dhamana kubwa sana kwani maendeleo ya sekta nyingine zote za kiuchumi na kijamii kwa kiasi kikubwa zinategemea ubora wa miundombinu mnayoijenga nyie. Rai yangu kwenu ni ile ile ambayo ipo kwenye azma yenu: kwamba kazi zenu muzifanye kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia muda na pesa iliyotengwa. Nimekuwa nasikitishwa sana na taarifa kwamba baadhi yenu mmekuwa hammalizi kazi ndani ya muda au mnafanya kazi chini ya kiwango cha ubora. Na lingine linalosikitisha ni baadhi yenu kukosa uaminifu. Naambiwa wapo baadhi yenu ambao baada ya kupewa kazi na kulipwa fedha za awali wamekuwa wakitokomea kusikojulikana na kutelekeza miradi. Mambo ya namna hii yanatia doa na kuharibu sifa za makandarasi. Naomba Bodi ya Usajili wa Makandarasi na nawasihi makandarasi kuonyana ili kuhakikisha vitendo hivi viovu havitokei. Muendelee kuelimishana, kusisitizana na kubanana ili kuhakikisha kuwa mnakuwa watu mnaoheshimu na kutimiza mikataba yenu: mnatekeleza kazi kwa wakati na kwa kiwango stahiki kwa mujibu wa mkataba. Ndugu Washiriki; Natambua kuwapo changamoto ambazo ziko nje ya uwezo wa makandarasi na kuathiri kazi mzifanyazo. Kwa mfano, kupanda kwa gharama za vifaa na mahitaji ya ujenzi kunakosababishwa na hali ya soko na uchumi wa ndani ya nchi au hata dunia. Haya ni mambo yanayozungumzika. Fanyeni hivyo, na naamini waliowapa kazi wataelewa. Nawahakikishieni utayari wa Serikali kwa ajili hiyo. Tunapata taabu sana pale ambapo chanzo cha hali hiyo ni makosa ya mkandarasi mwenyewe kuchelewa kutimiza wajibu wake kwa sababu za uzembe au uwezo mdogo. Inazua mivutano na hata kushitakiana. Vilevile, natambua kwamba wakati mwingine tatizo ni sisi tunaowapa kazi katika Serikali na sekta binafsi kuchelewa kuwalipa makandarasi kwa muda uliopangwa ili waweze kuendelea na kazi. Waajiri hatuna budi kutimiza ipasavyo wajibu wetu. Sisi katika serikali tunafanya jitihada kupunguza tatizo hili kwa upande wetu hasa pale ambapo sababu ni urasimu au uzembe wa watu. Kwa yale yahusuyo kuchelewa kupatikana fedha toka Hazina na wafadhili nayo pia tutayazungumza kuona namna ya kuyapunguza. Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Makandarasi; Naomba nichukue fursa hii kusisitiza mambo matatu: Jambo la kwanza, napenda kuwahimiza makandarasi, hasa makandarasi wadogo, kuungana na kufanya kazi kwa ubia ili kujiongezea uwezo. Hili ni jambo muhimu sana kwani miradi mikubwa ya ujenzi inahitaji uwezo mkubwa ambao makandarasi wadogo peke yao uwezo huo hawana na taabu kujenga nguvu hiyo. Lakini, makandarasi wadogo wakiunganisha nguvu zao watakazochangia zitawezesha kujenga uwezo wa kumudu kutekeleza miradi mikubwa. Natoa wito maalum kwa makandarasi wazalendo ambao wengi wao, taarifa inasema ni asilimia 85, ni wadogo kuupa uzito unaostahili wito wangu huu. Naamini mkifanya hivyo kilio chenu kwamba hampewi miradi mikubwa ya ujenzi kitakwisha. Naelewa hisia za wanaogawa kazi kwamba wanatazama uwezo wa makandarasi kwa kila kazi wanayotoa. Kwa vile makandarasi wazalendo walio wengi ni wadogo hawapewi miradi mikubwa. Ndiyo maana nasisitiza kuungana kwenu ili mjenge sifa za kupewa miradi mikubwa. Aidha, nawaomba mtumie fursa ya financial leasing kupata vifaa. Sherie ile imekusudiwa kuwawezesha watu kupata mitambo ya kufanyia shughuli. Naambiwa benki bado hazijatoa ushirikiano wa kutosha. Nitumie nafasi hii kuziomba benki kutoa ushirikiano unaostahili. Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanaotoa kazi kuwathamini na kuwaamini makandarasi wazalendo walio wakubwa na wadogo. Mimi naambiwa hata wale wakubwa wanapata taabu kupewa kazi. Wapeni kazi ili na wao wajenge uwezo. Hakikisheni mnaweka wahandisi washauri mahiri ili wasimamie vizuri kazi na kuhakikisha kiwango cha ubora kinachostahili kinafikiwa. Tusipojenga moyo wa kuwaamini na kuwapa kazi kamwe hawatakua na kuwa wakubwa. Watabakia kuwa wadogo milele. Hali hiyo haina maslahi kwa taifa. Tunapenda na makampuni ya Kitanzania nayo yaweze kutoka nje ya mipaka yetu na kuleta sifa na manufaa kwa taifa kama yafanyavyo makampuni ya nchi nyingine. Hatutafika hapo kama hatutachukua hatua za makusudi za kulea na kujenga makampuni ya wazalendo wetu. Si mengi lakini tukijisaidia mawili matatu hayatakosekana. Ndugu Mwenyekiti; Jambo la pili ambalo ningependa kulisisitiza leo ni matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya ujenzi. Ndugu Washiriki; Sote tunatambua kwamba dunia sasa inapita katika kipindi cha mabadiliko makubwa na ya haraka ya kiufundi na kiteknolojia. Ingawa teknolojia inayozungumziwa sana ni ile ya habari na mawasiliano, ukweli ni kwamba mabadiliko haya yapo katika nyanja zote pamoja na hii yenu ya ujenzi. Mabadiliko haya ya teknolojia ya ujenzi yana athari za namna mbalimbali kwa upande wa ufundi, ubora, ufanisi wa kazi pamoja na gharama. Ni dhahiri kabisa kwamba ujenzi wa majengo au uwekaji lami wa leo na hata muonekano wa barabara ya lami au za udongo ni tofauti sana na ule wa miaka ya 1980. Hivyo basi, rai yangu kwa makandarasi wote ni kwenda na wakati. Watumie ujuzi, maarifa na teknolojia za kisasa katika kazi zenu mzifanyazo. Msibaki nyuma kwa kutumia mbinu na maarifa ya miaka ya nyuma. Hamtaweza kumudu ushindani ambao ndiyo msingi mkuu wa kufanya kazi katika dunia ya leo na ndiyo matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Kukosa ufanisi na ubora kunaongeza gharama, hivyo kuwafanya washindwe kupata kazi. Mwenyekiti amezungumzia suala la kutumia makandarasi kwa majengo ya jamii. Sina tatizo nalo. Nami nalipenda, lakini mmejiuliza kwa nini wananchi wanaona bora watumie fundi mwashi wao badala ya mkandarasi? Ndugu Mwenyekiti; Suala la tatu ambalo ningependa kuliongelea ni suala la rushwa katika mchakato mzima wa utafutaji, upatikanaji na utekelezwaji wa miradi (zabuni) katika sekta ya ujenzi. Mdudu rushwa yupo hata katika sekta ya ujenzi pia. Sekta hii inatumia pesa nyingi na vishawishi vya kutafuta njia za mkato kwa waombaji na watoaji kazi ni vikubwa. Na hivyo kuwa kichocheo kimoja kikubwa cha rushwa. Penye rushwa kazi zimekuwa zikitolewa pasipo kuzingatia matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Makandarasi wasio na uwezo hupewa kazi au usimamizi wa kazi kuwa mbaya. Matokeo yake ni kazi kutokuwa na ubora wala uimara unaostahili. Wakati mwingine kazi huchelewa kukamilika na kusababisha watu kuchelewa au hata kukosa huduma hiyo na kuzua manung’uniko ya wananchi kwa Serikali yao. Wakati mwingine usalama wa watu na mali zao huwa hatarini na kuwatia hasara kubwa wenye miradi (Serikali au watu binafsi) na hivyo kupunguza kasi ya maendeleo ya taifa kwa ujumla. Bodi yenu, pamoja na Bodi zingine kama vile Bodi ya Usajili wa Wahandisi, inao pia wajibu mkubwa wa kudhibiti tatizo hili. Ni kwa heshima yenu na manufaa kwa taifa. Ndugu Mwenyekiti; Nimefurahi kwamba katika mkutano wenu mtajadili pia athari za mtikisiko wa uchumi wa dunia kwa sekta ya ujenzi. Uchumi wa dunia unapita katika kipindi kigumu. Tatizo limeanzia nchini Marekani na Ulaya, lakini sote tumeathirika. Kuelewa vizuri ukweli kuhusu mgogoro wa uchumi duniani na athari zake kwa uchumi wetu na shughuli za kila mmoja wetu ni jambo muhimu sana kwetu sote. Inatusaidia kujipanga vizuri kukabiliana na athari zake ikiwa ni pamoja na kujihami na kutumia fursa zake. Mheshimiwa Waziri, Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Washiriki; Kabla sijamaliza, napenda kuwapongeza wale wote waliopata tuzo za mwaka huu. Tunawapongeza kwa ufanisi wao. Naomba iwe changamoto kwa wengine wafanye vizuri mwakani. Mwisho kabisa, pamoja na yote niliyoyasema, naomba nimalizie kwa kuwaachia changamoto chache, ambazo nina uhakika mnaziweza: 1. Makandarasi wote ni muhimu wafanye kazi kwa kuzingatia usalama wa watu, kuweka mbele ubora wa kazi zao, na kuzingatia muda na gharama iliyopangwa. 2. Makandarasi wote ni lazima wafanye kazi kwa kuzingatia utunzaji na uendelezaji mazingira. 3. Makandarasi wote wahakikishe wanafanya kazi zao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria husika za nchi. 4. Makandarasi wote wawe ni chanzo na chachu ya utoaji na uboreshaji ajira kwa wananchi wa eneo husika la mradi na kwa Watanzania kwa ujumla. 5. Makandarasi wote wawe wepesi na mfano katika kuchangia shughuli za hisani (Corporate Social Responsibility) kama mchango wao na utambuzi wa jamii ambapo miradi yao ipo. Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Washiriki, Mabibi na Mabwana; Baada ya kusema maneno haya mengi, sasa natamka kwamba Mkutano wa Mashauiriano kwa mwaka 2009 umefunguliwa rasmi. Nawatakia mkutano wenye mafanikio mema. Nasubiri kwa hamu matokeo yake. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. HOTUBA YA RAIS: UZINDUZI WA KIVUKO CHA MV. MAGOGONITarehe 4 Juni 2009
Awali ya yote, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunialika kuja kujumuika nanyi hapa katika uzinduzi wa kivuko kipya cha Mv. Magogoni.Nawapongeza sana wananchi wa Kigamboni na wa jiji la Dar es Salaam kwa jumla kwa kupata kivuko kipya kiitwacho MV. Magogoni. Kivuko hichi kipya, kikubwa na cha kisasa tumekinunua kutoka Ujerumani kwa gharama ya shilingi 8.5. bilioni. Kimetatua tatizo kubwa lililokuwa linawasumbua watu waliokuwa wanavuka kutoka au kwenda Kigamboni. Kwa muda mrefu, wananchi wa Kigamboni wamekuwa wakipata adha ya usafiri, maisha yao kuwa hatarini na usalama wa mali zao kuwa mashakani. Vivuko vilivyokuwepo MV. Alina na MV. Kigamboni vilikuwa vimechakaa sana hivyo kushindwa kufanya kazi ipasavyo. Kwa kweli vilikuwa tishio kwa kila hali. Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005, Chama cha Mapinduzi kiliahidi kupitia Ilani yake kutatua tatizo la vivuko kadhaa nchini, kimojawapo kikiwa hiki cha Kigamboni. Leo hii tunasherehekea kutimia kwa ahadi yetu kwa wananchi wa Dar es Salaa hasa wale waishio na waendao Kigamboni. Kadhalika tumeshatimiza ahadi kwa wananchi wa Mwanza kwa kivuko cha Busisi (MV. Misungwi), kivuko cha Kisiwa cha Kome (MV. Kome) na kivuko cha kati ya Bugorora na Ukara (MV. Nyerere). Kwa wananchi wa Ruvuma kuna kivuko cha MV. Ruhuhu na wa Morogoro kivuko cha mto Kilombero. Kivuko hiki tunachokizindua rasmi leo ndicho kikubwa kuliko vivuko vyote nchini. Kina uwezo mkubwa wa kubeba tani 500 yaani Magari 60 na abiria 2000 kwa wakati mmoja. Kwa kuwa na kivuko hiki tatizo la usafiri sasa siyo gumzo tena. Ifikapo mwezi Septemba, 2009 tatizo litakuwa limekwisha kabisa pale kivuko cha MV. Kigamboni kitakapoanza kazi. Hivi sasa kivuko hicho kinafanyiwa matengenezo makubwa kukirudisha katika kiwango cha juu cha ubora. Kadhalika kule Bususi, Mwanza nako matengenezo ya kivuko cha MV. Sengerema yatakapokamilika shughuli ya uvushaji watu kati ya Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria itakuwa imeimarika sana. Ndugu Wananchi, Nimefurahi kusikia kuwa ujenzi wa Kivuko Mv. Magogoni umefanyikia hapa Dar es salaam eneo la Bandari na kuweza kuwapatia ajira vijana 30 ambao wamejifunza na kupata maarifa na ufundi mpya wa ujenzi wa vivuko na hata maboti. Ninaamini kwa uzoefu walioupata wataweza kujiajiri wenyewe kwa kujenga vivuko na boti ndogondogo za uvuvi ili kujipatia riziki na kuboresha hali ya maisha yao. Serikali itaendelea na utaratibu huu wa kujenga vivuko hapa nchini ili kutoa huduma nzuri ya usafiri wa majini na kuendeleza teknolojia ya ufundi wa kutengeneza vivuko hapa nchini, na kukuza ajira kwa vijana wetu. Ndugu wananchi, Ziko sehemu nyingi za nchi yetu ambako kufikika kwake ni kwa vivuko tu. Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa vivuko vyote nchini vinakuwa vya uhakika na salama kwa matumizi ya wananchi kwa kuvikarabati na kununua vipya pale vinapohitajika kadri uwezo wa bajeti ya serikali unavyoruhusu. Katika kutekeleza hayo, Serikali kwa sasa inakarabati vivuko viwili vya Mv. Kigamboni hapa Dar es Salaam, na Mv. Sengerema huko Mwanza. Aidha, tumenunua vivuko vipya sita vya Kilombero huko Morogoro, Kivuko cha Mv. Nyerere kinachohudumia kati ya Bugorora na Ukara Mkoani Mwanza, Mv. Ruhuhu Mkoani Ruvuma, Mv. Misungwi kinachohudumia kati ya Kigongo hadi Busisi huko Mwanza na Mv. Kome II kinachofanya kazi kati ya Kisiwa cha Kome kwenda Nyakalilo. Vilevile, tutanunua vivuko vipya vya Musoma kwenda Kinesi Mkoani Mara ambapo wananchi wa Kinesi watakwenda Musoma mjini kwa kutumia kivuko kwa muda wa dakika 30 badala ya kuzunguka Kilometa 54, pia tunanunua vivuko vingine vipya vya Rugezi hadi Kisorya Wilayani Ukerewe, Utete mkoani Pwani na Pangani mkoani Tanga. Vilevile, katika mipango ya miaka mitatu ijayo, Serikali inatarajia kununua vivuko vifuatavyo kuanzia 2009/10: 1. Kivuko cha tani 50 katika maeneo ya Kilambo - Mtwara. Kivuko hiki kitarahisisha usafiri eneo la mwambao wa kati ya Mtwara Tanzania na Msumbiji 2. Kivuko cha tani 50 kitakachotumika kati ya Msanga Mkuu na Mtwara Mjini ambapo kitapunguza usumbufu wa wananchi kuzunguka Km 20 kufika Mtwara. 3. Kivuko cha Mto Rusumo – Ngara Kagera ambapo kitapunguza Km 60 za kuzunguka kuja Bukoba Mjini. 4. Kivuko cha Kyela – Itungi Port wananchi watatumia nusu saa kusafiri kwa kivuko badala ya kuzunguka kwa Km 70 kufika Kyela. Ndugu wananchi, Kuna sehemu ambazo tunatumia vivuko kwa sababu ya kujenga madaraja haiwezekani kwa jinsi maumbile yake yalivyo. Lakini zipo sehemu ambazo tunatumia vivuko lakini madaraja yanawezekana kujengwa. Tunachelewa kujenga madaraja kwa sababu ya gharama kubwa na uwezo wetu mdogo wa fedha. Tunayo dhamira ya kujenga madaraja kidogo kidogo katika sehemu hizi. Moja ya madaraja ambayo tumeshafanya uamuzi wa dhati kabisa kujenga ni Daraja la Kigamboni. Mipango ya ujenzi wa daraja hili imekuwapo tangu uhuru. Lakini sasa tumedhamiria kufanya. Tumeahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM Ibara ya 44 (f) kwamba, katika kipindi cha miaka mitano tuwe tumeanza maandalizi ya ujenzi wa daraja hili. Nafurahi kwamba tutatimiza ahadi hiyo. Na tutafanya hivyo kwa kushirikiana na wenzetu wa sekta binafsi. Tuko kwenye hatua nzuri za maandalizi. Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lipo kwenye mchakato kumpata Mtaalam Mshauri ili atayarishe nyaraka za zabuni. Matumaini yetu ni kwamba, ifikapo mwezi Septemba mwaka huu, nyaraka hizo zitakuwa tayari. Mambo yote yakienda kama yalivyopangwa, basi ujenzi wa daraja unaweza kuanza katika mwaka wa fedha wa 2010/2011. Daraja hili litafungua kwa kiasi kikubwa fursa za uchumi na uwekezaji huko Kigamboni. Vilevile, kwa sasa, tunafanya usanifu wa ujenzi wa daraja tuliloliahidi kwenye ibara ya 44 (i) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM wa 2005, yaani Daraja la Mto Kilombero ili kuunganisha Wilaya za Kilombero na Ulanga. Ndugu wananchi, Hata hivyo, kujenga daraja kuvuka ng’ambo pekee hakutoshi kama barabara za Kigamboni haziko katika hali nzuri. Kwa kutambua hilo tunajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kivukoni hadi Mjimwema mpaka Kongowe. Barabara nyingine tutakayojenga kwa lami ni ya kutoka Kivukoni hadi Tungi na nyingine ni ile ya kutoka Mjimwema hadi Pembamnazi. Wakati tunajenga barabara hizi kwa lami, tutaendelea kuimarisha barabara nyingine za Kigamboni, kama ile ya Tungi hadi Kibada. Ndugu wananchi, Ukiacha hili la Kivuko ambalo tumelitimiza na barabara za Kigamboni, Serikali inaendelea na jitihada za kupunguza matatizo ya ya usafiri na usafirishaji katika Jiji la Dar es Salaam. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika kujaribu kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Dar es Salaam. Kwa ajili hiyo, zipo barabara ambazo tunazifanyia ukarabati mkubwa ili zirudi katika hali yake ya zamani, kama tufanyavyo kwa barabara ya Mandela. Baadhi tunazijenga upya na kuzipanua kama ilivyo kwa barabara ya Sam Nujoma na barabara ya Kilwa. Nyote ni mashahidi wa kazi inayoendelea kufanyika katika barabara hizo. Vilevile ziko barabara kadhaa za Dar es Salaam ambazo hivi sasa ni za udongo ambazo tumeamua tutazijenga kwa kiwango cha lami. Nia yetu kuu ni kupunguza msongamano katika baadhi ya mabarabara kwa kutoa fursa kwa magari kuchepukia barabara hizo. Tumekwishatoa kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa barabara hizi. Baadhi ya barabara hizo ni pamoja na zifuatazo: 1. Barabara ya kutoka Ubungo Bus Terminal hadi Kigogo Roundabout, na kutoka Kigogo Roundabout hadi Mtaa wa Twiga Jangwani. Maombi yangu ni kwamba wasiue viwanja vya michezo vya Jangwani. Nimeambiwa kuwa mikataba ya ujenzi wa barabara hizi itasainiwa wakati wowote wiki ijayo na ujenzi kuanza mara moja. 2. Barabara nyingine ni ile ya kutoka Tabata Dampo hadi Kigogo; 3. Vilevile iko barabara ya kutoka Ubungo Maziwa hadi Mabibo External; 4. Barabara ya kutoka Jet Club hadi Vituka hadi Davis Corner ya umbali wa kilomita 12; 5. Barabara ya kuanzia Mbezi Mwisho hadi Barabara ya Nyerere Ukonga Banana kupitia Malamba Mawili na Kinyerezi. Barabara hii itawezesha magari yanayotoka viwandani maeneo ya Nyerere Road kuweza kuanza safari za mikoani au nchi jirani bila kupitia Ubungo. 6. Barabara ya kutoka Tegeta Kibaoni hadi Mbezi Mwisho (Morogoro Road) kupitia Goba. Barabara hii itawawezesha wachukuzi wa saruji kutoka kiwandani Wazo Hill kwenda mikoani au nchi jirani bila kupitia mjini. Vilevile itawezesha wakazi wengi wa maeneo ya Bagamoyo Road, Tegeta na Mbweni kuweza kusafiri mikoani bila kupitia mjini. 7. Tunao mpango wa kutengeneza kwa lami barabara kutoka Tangi Bovu hadi Goba 8. Vilevile tunao mpango wa kupanua njia mbili kipande cha barabara kutoka njia panda ya Morocco hadi Kawe kuungana na barabara ya Bagamoyo kupitia Shoppers Plaza, kupitia Mikocheni na Mlalakua ili kupunguza msongamano mkubwa wa kipande kile cha barabara. Pia kuunganisha kipande cha kutoka Tume ya Sayansi hadi Msasani kwa Mwalimu Nyerere kwa barabara ya njia mbili. 9. Pia barabara ya Kimara Kinguruwe hadi Mabibo External nayo tutaijenga kwa lami. Barabara hii ya kilomita 9 itawezesha watu kupita kuja na kutoka mjini bila kupitia Ubungo; 10. Vilevile, ipo mipango ya kutengeneza kwa lami barabara ya Kimara Baruti hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Msewe na Changanyikeni. 11. Tumefanya mazungumzo mazuri na Serikali ya Japan wakati wowote tutapata majibu kuhusu utoaji fedha kwa ajili wa upanuzi wa barabara ya kutoka njia panda ya Morocco Road hadi Tegeta Kibaoni ambayo itapunguza sana msongamano wa magari Jijini. Ndugu wananchi, Nimeona niwape taarifa ya barabara hizi ili mjue hatua tunazochukua kupunguza tatizo la usafiri Dar es Salaam. Usalama wa Vyombo vya Majini Ndugu wananchi, Hali ya usalama wa vyombo vya majini imekuwa siyo ya kuridhisha hata kidogo. Matukio ya ajali za vyombo vya majini hapa nchini yamekuwa mengi mno. Katika kipindi cha kuanzia Januari, 2006 hadi Desemba 2008 yamekuwepo matukio 28 ya ajali zilizo sababisha vifo vya watu 149 na 240 kuokolewa. Majuzi tena kumetokea ajali ya Meli ya Mv. Faith iliyopinduka katika Bandari ya Malindi kule Zanzibar. Tathmini zinaonyesha kuwa ajali hizo zimekuwa zinasababishwa na ubovu wa vyombo unaochangiwa na umri mkubwa na matengenezo yasiyoridhisha, makosa ya kibinadamu na hali mbaya ya hewa. Wakati mwingine pia uelewa mdogo wa umuhimu na matumizi ya vifaa vya kuokolea umechangia vifo vya watu. Serikali iliunda SUMATRA kwa nia ya kuboresha usimamizi wa uendeshaji wa vyombo vya majini ili kuongeza usalama wa usafiri majini. Tunaipongeza SUMATRA kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imekuwa inafanywa tangu kuundwa kwake mpaka sasa. SUMATRA imeweka maafisa wasimamizi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mwanza, Bukoba, Sumbawanga, Kigoma na Dar es Salaam. Hata hivyo, lazima SUMATRA waongeze udhibiti wa vyombo vinavyosafiri majini. Wawe makini zaidi katika kusimamia ubora wa vyombo hivyo, ujuzi wa manahodha na wafanyakazi wake, ubora wa huduma stahiki kwa abiria ikiwamo zile za kuokolea abiria panapotokea ajali. Aidha SUMATRA iendelee kutoa mafunzo kwa wamiliki na waendesha vyombo vya usafiri majini ili kuwaongezea ufahamu juu ya umuhimu wa kuzingatia taratibu na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa vyombo hivyo. Ndugu wananchi, Katika kuimarisha uwezo wetu wa kuzuia na kukabiliana na majanga kwenye maji, Serikali imejenga mnara wa kuongozea meli katika eneo la Magogoni ambao una kituo cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji pamoja na kuratibu matukio ya uharamia baharini. Kituo hiki kimezinduliwa mwezi Machi, 2009 na kwa muda mfupi wa uwepo wake, kimeweza kuratibu zoezi la utafutaji na uokoaji wa meli ya Comoro iliyopata ajali ikiwa safarini kutoka Dar es salaam kwenda Comoro tarehe 16 Aprili, 2009. Katika zoezi hilo watu 77 waliokolewa. Ndugu wananchi, Kabla sijamaliza, naomba niongelee uvumi ambao umeenea sana ndani ya jamii yetu, hasa kwa wakazi wa Kigamboni. Kumekuwa na upotoshaji mkubwa kwamba eneo zima la Kigamboni limeuzwa kwa wawekezaji. Wapo wanaodai kuwa Kigamboni imeuzwa kwa watu maarufu wa Marekani na wapo wanaodai kwamba imeuzwa kwa watu maarufu kutoka Uarabuni. Mwanzoni niliposikia maneno hayo niliyapuuza. Lakini nikagundua kuwa yameenea sana na yanaaminiwa na watu wengi hata wale ambao ungedhani wana uelewa wa juu wa mambo. Nikamuagiza Waziri wa Ardhi atoe ufafanuzi. Ningependa nami kurudia kwamba hakuna ukweli kabisa katika uvumi huo. Ninachokijua mimi ni kuwa Jiji Dar es Salaam likishirikiana na Serikali Kuu (Wizara ya Adhi, Nyumba na Makazi) inao mpango kabambe wa kuufanya Kigamboni kuwa Mji Mpya. Hii ni kwa maana ya kwamba uwe umepangwa na kujengwa kisasa. Nia ni nzuri ya kuendeleza Kigamboni na jiji la Dar es Salaam kwa jumla hasa sasa ambapo kutajengwa daraja hivyo kushawishi watu wengi zaidi kupenda kuhamia na kuishi huko. Tatizo kubwa la Dar es Salaam ni kuwa na nyumba nyingi kujengwa maeneo yasiyopimwa na kupangwa vizuri. Hali hii haikubaliki, tusiiache iendelee hivi. Na tusiiache Kigamboni nayo ikawa hivyo. Mwelekeo huo tayari upo. Ndiyo sababu ya uamuzi huo wa Jiji na Wizara ya Ardhi ambao nia yake ni njema, naomba tuwape ushirikiano na msaada unaostahili. Ndugu Wananchi, Naomba sasa nimalize kwa kuwakumbusha wenzetu wa Wizara na hasa TEMESA kuhakikisha kuwa kivuko hiki kunatunzwa ipasavyo. Kinafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kwa mujibu wa ratiba yake. Hamzidishi magari, abiria na mizigo kupita uwezo unaostahili. Tukifanya hayo kitadumu na kutuhudumia kwa miaka mingi kama ilivyokusudiwa. Tuukumbuke daima msemo wa Waswahili usemao “Kitunze Kidumu” na Kitunze Kikutunze” Tusifanye kinyume chake. Baada ya kusema hayo, sasa niko tayari kwa uzinduzi wa kivuko hiki kipya cha Mv. Magogoni. ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA HOTUBA YA RAIS, UZINDUZI RASMI WA UJENZI WA BARABARA YA SINGIDA – BABATI – MINJINGUMnamo tarehe 04 Agosti 2009, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua rasmi ujenzi wa barabara ya Singida - Babati - Minjingu.
IFUATAYO NI HOTUBA YA RAIS: Nawashukuruni sana kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika sherehe hii ya kuzindua ujenzi wa barabara ya Singida – Babati hadi Minjingu. Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ningependa kumkaribisha rasmi Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Sipho Moyo. Tunakushukuru sana kwa kuitikia mwaliko wetu kuja kujumuika nasi katika hafla hii. Dkt Moyo karibu sana. Ndugu Wananchi, Kama alivyotangulia kusema Waziri wa Miundombinu, barabara hii ina umuhimu mkubwa kwa nchi yetu na majirani zetu pia. Majirani zetu wa Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na hata Uganda watapata njia mbadala ya kusafirishia mizigo yao kutoka bandari ya Tanga. Bandari ya Tanga ikitumika ipasavyo,itasaidia sana kupunguza msongamano wa meli na makontena katika bandari ya Dar es Salaam. Haya yatawezekana tu pale tutakapokuwa na barabara nzuri na imara. Tukiwa na barabara nzuri tutakuwa na fursa nzuri ya kufanya biashara na majirani zetu hawa. Barabara nzuri ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo kwa kipindi kirefu itaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wetu. Tukiwa na barabara nzuri ni wazi kuwa Wananchi wetu watapata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu. Kwa upande mwingine, mazao yao yatafika sokoni kwa wakati na hivyo wakulima watapata bei nzuri kwa mazao yao. Barabara nzuri ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa maeneo ya mijini na vijjijini. Ni ukweli ulio dhahiri kuwa tukiwa na barabara imara, shughuli za utalii zitaongezeka na huduma za afya, elimu na utawala zitaimarika pia. Ndugu Wananchi, Kwa kuzingatia ukweli huu, Serikali inaendelea kutenga fedha katika bajeti yake na kufanya mazungumzo na Wahisani mbalimbali ili kupata fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Ndugu Wananchi, Tumearifiwa na Katibu Mkuu kuwa ujenzi wa barabara hii utagharimu shilingi bilioni 210. Hizi si fedha kidogo. Kwa miaka mingi Benki ya Maendeleo ya Afrika imekuwa ikitoa misaada kugharamia ujenzi wa barabara zetu kwa nia ya kuimarisha ukuaji wa uchumi wetu, kuondoa umaskini na kuboresha hali ya maisha ya watu wetu. Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania kupitia kwa Mwakilishi wa Benki kuishukuru kwa dhati kabisa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa misaada ambayo imekuwa ikiitoa kwa nchi yetu. ADB ni mshirika wa kweli wa maendeleo ya nchi yetu. Ndugu Wananchi, Mbali ya kuchangia kukuza uzalishaji wa mazao ya kilimo, njia imara za usafishaji zinasaidia kufungua fursa mpya za uwekezaji katika maeneo mengine ya uchumi. Miradi ya ujenzi wa barabara huko vijijini imekuwa ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato kwa wananchi wetu hali ambayo inasaidia kupunguza wimbi la vijana ambao ndio nguvu kazi kukimbilia mijini. Pamoja na juhudi zinazoelekezwa katika ujenzi wa barabara kuu, wakati umefika kuongeza juhudi katika ujenzi wa barabara za mikoa na wilaya ili kuchochea maendeleo vijijini. Ndugu Wananchi, Kwa bahati mbaya uboreshaji wa barabara zetu unaonekana kuambatana na ongezeko la ajali za barabarani. Takwimu zinaonyesha kuwa mikoa yenye barabara nzuri za lami ndiyo inayoongoza kwa kuwa na viwango vikubwa vya ajali za barabarani. Taarifa zinaonyesha kuwa ajali nyingi zinachangiwa na mwendo kasi, ulevi wa madereva, uzembe wa madereva kutozingatia sheria za barabarani na wizi wa alama za barabarani ambazo hutoa tahadhari kwa madereva. Ni hivi majuzi tu wananchi ishirini na nane walipoteza maisha katika ajali mbaya nay a kutisha iliyotokea wilayani Korogwe mkoani Tanga. Serikali haitavumilia kuona hali hii ikiendelea. Wizara ya Mambo ya Ndani iwachukulie hatua kali madereva wote watakaobainika kusababisha ajali kwa sababu za uzembe unaotokana na mwendo kasi, ulevi ama kutozingatia sheria za barabara. Aidha, viongozi wa mikoa, wilaya na vijiji zinapopita barabara za lami wahakikishe kuwa wote wanaohujumu miundombinu ya barabara kwa kuiba alama za barabara wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Endapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake, kwa nafasi yake, nina imani tunaweza kukomesha kabisa ajali ambazo zinaweza kuepukwa. Ndugu Wananchi, Bado tunalo tatizo sugu kwa baadhi ya madereva na wamiliki wa magari ya kusafirisha mizigo na abiria kuzidisha uzito wa mizigo katika magari yao. Tabia hii inachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu barabara zetu. Barabara ambayo kwa kawaida ingedumu kwa miaka 15, inaharibika na kuhitaji matengenezo makubwa baada ya takriban miaka minane tu. Ni muhimu kwa Wizara ya Miundombinu kwa kushirikiana na Wakala wa barabara, (TANROADS) kuhakikisha kuwa zoezi la upimaji na uthibiti uzito wa magari linaendeshwa kwa umakini mkubwa. Endapo mizani iliyopo itatumiwa kwa lengo lililokusudiwa, nina imani barabara zitalindwa kutokana na uzidishaji wa uzito wa magarizetu na hivyo kupunguza gharama za matengenezo na ukarabati wa barabara. Ndugu wananchi, Uzoefu umeonyesha kuwa ujenzi wa barabara za lami unaongeza na kurahisisha mawasiliano kati ya sehemu moja hadi nyingine na hivyo kuongeza shughuli za kijamii na kiuchumi. Kwa bahati mbaya, hali hii inaonekana kuchangia sana ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Sasa hivi kuna ongezeko kubwa la watu kutoka maeneo mbalimbali wanaofuata ajira katika mradi huu. Napenda kutoa wito kwa Wananchi wote kuzingatia ushauri na maelekezo yanayotolewa na wataalamu kuhusu njia sahihi za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu hatari. Kuna umuhimu wa kujiepusha na vitendo au mazingira hatarishi yanayoweza kuchangia maambukizi ya ugonjwa huu ambao hadi sasa haujapata kinga wala tiba. Ndugu wananchi, Naomba nimalize hotuba yangu kwa kuwashukuru tena wenzetu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kukubali kwao kutuunga mkono katika maeneo mengi ya maendeleo hususan uimarishaji wa Miundombinu ya usafiri nchini. Aidha nawashukuru sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia tukio hili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Waheshimiwa Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA. The Global Aviation Safety Roadmap Workshop
On behalf of the Government of the United Republic of Tanzania and on behalf of the East African Community (EAC) Ministers responsible for civil aviation, it is my great privilege and honour to welcome you all to this Global Aviation Safety Roadmap Workshop for the East African Community Partner States and the regional aviation safety oversight agency i.e. - the Civil Aviation Safety and Security Agency (CASSOA), which is being held in this beautiful City of Arusha. The Government of United Republic of Tanzania is grateful to the organizers of this workshop: the International Civil Aviation Organization (ICAO) and Industry Safety Steering Group (ISSG) for having chosen Tanzania and Arusha in particular, as your venue for this important workshop. For those of you coming from outside the East African Community, the city of Arusha hosts the Headquarters of the East African Community which currently comprises of five Partner States of Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda and Tanzania.... Opening of the International Expert Review Meeting on Regional Climate Outlook Forums
On behalf of the Government of the United Republic of Tanzania, it is my great privilege and honour to welcome you all to this INTERNATIONAL EXPERT REVIEW MEEING ON REGIONAL CLIMATE OUTLOOK FORUMS, which is being held in this beautiful City of Arusha. The Government of the United Republic of Tanzania is grateful to the organizers of this meeting for having chosen Tanzania and Arusha in particular, as your venue for this important Meeting. Im told there are more than 50 scientists coming from different countries globally. For those of you coming from outside the East African Community, the city of Arusha hosts the Headquarters of the East African Community which currently comprises of five Partner States of Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda and Tanzania. In addition, Arusha lies at the centre of Tanzanias famous tourist attractions including Mount Kilimanjaro, Ngorongoro and Serengeti while Zanzibar is only a short distance away. Therefore, it is my sincere hope that you will find the environment in Arusha conducive for your work programme and conclude your business as scheduled... |
More Speeches and Statements
- HOTUBA YA RAIS: MKUTANO WA MASHAURIANO KWA MWAKA 2009 WA BODI YA USAJILI WA MAKANDARASI (CRB)
- HOTUBA YA RAIS: UZINDUZI WA KIVUKO CHA MV. MAGOGONI
- HOTUBA YA RAIS, UZINDUZI RASMI WA UJENZI WA BARABARA YA SINGIDA – BABATI – MINJINGU
- The Global Aviation Safety Roadmap Workshop
- Opening of the International Expert Review Meeting on Regional Climate Outlook Forums
- Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Katika Uzinduzi Rasmi Wa Ujenzi Wa Barabara Ya Mbeya - Lwanjilo
- Speech by the Minister on Challenges and Opportunities for Private Sector Participation
- Speech by the Minister at the High Level Meeting on Almaty Programme of Action
- Speech by the Minister on Multinational Tanzania-Rwanda-Burundi Railway Project
- Opening Speech by the Minister for Infrastructure Development, on Construction Industry Forum
