Home | The Ministry | Service Charter | Projects | Policies | Publications | News & Events | Speeches | Tenders | FAQ | Links | Contact Us
image
Hon Dr.Shukuru Kawambwa(MP) Minister of Infrastructure Development
Hon. Hezekiah Ndahani Chibulunje (MP) Deputy Minister

image
Eng. Omar Chambo, Permanent Secretary
rss
Subscribe to RSS News
Comments / Maoni

Ministry of Infrastructure Development

Its mission is to facilitate provision of an economic, safe and reliable construction industry, transport and services, meteorology, electrical and mechanical services, government buildings and stores that meet the needs of the public through development and implementation of appropriate sector policies, strategies and standards.

Speeches and Statements

HOTUBA YA RAIS: MKUTANO WA MASHAURIANO KWA MWAKA 2009 WA BODI YA USAJILI WA MAKANDARASI (CRB)

MKUTANO WA MASHAURIANO - CRB 2009
Kwanza kabisa, nakushukuru wewe Waziri na Bodi ya Usajili wa Makandarasi kwa kunikaribisha na kunishirikisha kwenye mkutano huu muhimu. Nawashukuru kwa burudani kutoka vijana wa THT.
Mwaliko wenu huu umenipa fursa ya kukutana na kuzungumza na wadau wa shughuli ya ukandarasi hapa nchini watu ambao ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu.
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi, Ndugu Msajili wa Makandarasi;

Napenda kuwapongeza kwa mambo mawili. Kwanza, kwa kuwa na utaratibu huu mzuri wa mikutano ya mashauriano kati ya Bodi ya Usajili wa Makandarasi na wadau wa sekta ya ujenzi nchini. Hii inadhihirisha kwamba Bodi ipo makini, inatambua wajibu wake na iko tayari kuutekeleza. Nafurahi kwamba mwaka huu mmechagua jambo muafaka kuwa mada kuu ya mkutano wenu. Kuzungumzia suala la upatikanaji wa thamani ya fedha kuwa jambo la msingi katika kuwa na miundombinu endelevu na kupunguza umasini au kwa lugha ya kigeni (value for money in construction: a key for sustainable infrastructure delivery and poverty reduction) ni jambo la msingi.

Pili, nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kusimamia ubora wa kazi za makandarasi nchini. Nimesikia maelezo ya Mwenyekiti wa Bodi pamoja na maelezo ya Msajili na nimeridhika na kufurahishwa na jitihada mnazofanya katika kusimamia, kuratibu na kuwaendeleza makandarasi kwa nia ya kuwalinda wateja wao na watumiaji wa huduma zinazotolewa na makandarasi. Aidha nafurahi kwamba kwa kufanya hivyo, mnahakikisha kuwa kazi iliyofanywa inalingana na thamani ya pesa (value for money) iliyotumika katika miradi iliyojengwa. Nimefarijika sana na hatua zinazofanywa na Bodi yenu katika kushughulikia makandarasi wasiotimiza ipasavyo wajibu wao ama kwa kukosa uwezo au kwa uzembe.

Kujenga jengo linalobomoka kabla ya kwisha, au daraja linalopata nyufa miezi mitano baada ya kutumika au kujenga barabara ambayo lami huanza kubanduka kabla barabara haijesha au mradi kuchukua miaka mingi kwisha ndo vinavyoivunjia heshima shughuli ya ukandarasi na taaluma nzima ya uhandisi na usanifu.
Mheshimiwa Waziri, Ndugu Washiriki;

Nimetiwa moyo sana kusikia jitihada za Bodi za kuwajengea uwezo makandarasi. Nawapongeza sana kwa kubuni wazo zuri la kuanzisha Mfuko wa Makandarasi, ambao utawasaidia makandarasi wadogo kwa kuwapatia Dhamana ya Kuombea Kazi (Bid Bond) na Dhamana ya Malipo ya Awali (Advance Payment Guarantees).
Pia, mmefanya uamuzi wa busara wa kuanzisha Mpango Endelevu wa Mafunzo ya Makandarasi ili kuinua uwezo wa makandarasi katika nyanja zote zinazohusiana na huduma hii muhimu.
Napenda nichukue fursa hii kuwahakikishia kuwa Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na Bodi ya Usajili katika kujenga msingi imara wa shughuli za ukandarasi hapa nchini. Ni matumaini yangu kuwa makandarasi mtatumia ipasavyo fursa hizi kwa manufaa yenu binafsi, kwa manufaa ya sekta na Taifa kwa ujumla.

Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Washiriki;
Nimeridhishwa na maelezo ya Mwenyekiti na Msajili wa Bodi, kwamba dukuduku nilizokuwa nazo kuhusu mwenendo wa huduma ya ukandarasi zinafanyiwa kazi. Kwahiyo, leo nitakuwa na machache sana ya kuzungumza.

Kwanza, naomba nianze kwa kusema kwamba, kama mnavyofahamu, serikali ni mdau na mtumiaji mkubwa wa huduma za makandarasi. Sisi katika Serikali tunatambua umuhimu wa pekee wa makandarasi kwa maendeleo ya Taifa letu. Miundombinu ya aina zote, barabara, reli, viwanja vya ndege, mifumo ya maji, majengo mbalimbali ya Serikali, makampuni na watu binafsi, migodi, viwanda, minara ya mawasiliano, n.k yote hayo ni matokeo ya kazi za makandarasi.

Ni dhahiri kuwa ubora na ufanisi wa kazi za makandarasi ni muhimu sana katika kujenga na kusukuma mbele maendeleo ya Taifa letu. Ndio maana nafurahishwa na jitihada zenu za kuimarisha ubora na ufanisi wa kazi za makandarasi. Katika kipindi hiki, ambapo Serikali imetenga kiasi kikubwa cha bajeti yake kwa ajili ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, maji, umeme, elimu, afya n.k. suala la ubora wa kazi za makandarasi ni muhimu sana kwetu sisi katika Serikali. Hali kadhalika mwekezaji katika sekta binafsi na miradi na watu binafsi
Jitihada zote za Serikali kuwekeza kwenye miundombinu pamoja na sekta binafsi na watu binafsi haziwezi kuwa na manufaa yeyote yale kama kazi zitakayofanywa hazitafikia viwango vya ubora vinavyohitajika. Dhamana ya kuhakikisha kuwa Serikali na kila mwekezaji anapata thamani ya fedha anayotumia katika miradi ya ujenzi ni yetu sote: nyie Makandarasi na sisi tunaowapa kazi katika Serikali sekta binafsi.

Ndugu Makandarasi;
Ninyi mnayo dhamana kubwa sana kwani maendeleo ya sekta nyingine zote za kiuchumi na kijamii kwa kiasi kikubwa zinategemea ubora wa miundombinu mnayoijenga nyie. Rai yangu kwenu ni ile ile ambayo ipo kwenye azma yenu: kwamba kazi zenu muzifanye kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia muda na pesa iliyotengwa.

Nimekuwa nasikitishwa sana na taarifa kwamba baadhi yenu mmekuwa hammalizi kazi ndani ya muda au mnafanya kazi chini ya kiwango cha ubora. Na lingine linalosikitisha ni baadhi yenu kukosa uaminifu. Naambiwa wapo baadhi yenu ambao baada ya kupewa kazi na kulipwa fedha za awali wamekuwa wakitokomea kusikojulikana na kutelekeza miradi. Mambo ya namna hii yanatia doa na kuharibu sifa za makandarasi. Naomba Bodi ya Usajili wa Makandarasi na nawasihi makandarasi kuonyana ili kuhakikisha vitendo hivi viovu havitokei. Muendelee kuelimishana, kusisitizana na kubanana ili kuhakikisha kuwa mnakuwa watu mnaoheshimu na kutimiza mikataba yenu: mnatekeleza kazi kwa wakati na kwa kiwango stahiki kwa mujibu wa mkataba.

Ndugu Washiriki;
Natambua kuwapo changamoto ambazo ziko nje ya uwezo wa makandarasi na kuathiri kazi mzifanyazo. Kwa mfano, kupanda kwa gharama za vifaa na mahitaji ya ujenzi kunakosababishwa na hali ya soko na uchumi wa ndani ya nchi au hata dunia. Haya ni mambo yanayozungumzika. Fanyeni hivyo, na naamini waliowapa kazi wataelewa. Nawahakikishieni utayari wa Serikali kwa ajili hiyo. Tunapata taabu sana pale ambapo chanzo cha hali hiyo ni makosa ya mkandarasi mwenyewe kuchelewa kutimiza wajibu wake kwa sababu za uzembe au uwezo mdogo. Inazua mivutano na hata kushitakiana.

Vilevile, natambua kwamba wakati mwingine tatizo ni sisi tunaowapa kazi katika Serikali na sekta binafsi kuchelewa kuwalipa makandarasi kwa muda uliopangwa ili waweze kuendelea na kazi. Waajiri hatuna budi kutimiza ipasavyo wajibu wetu. Sisi katika serikali tunafanya jitihada kupunguza tatizo hili kwa upande wetu hasa pale ambapo sababu ni urasimu au uzembe wa watu. Kwa yale yahusuyo kuchelewa kupatikana fedha toka Hazina na wafadhili nayo pia tutayazungumza kuona namna ya kuyapunguza.

Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Makandarasi;
Naomba nichukue fursa hii kusisitiza mambo matatu:
Jambo la kwanza, napenda kuwahimiza makandarasi, hasa makandarasi wadogo, kuungana na kufanya kazi kwa ubia ili kujiongezea uwezo. Hili ni jambo muhimu sana kwani miradi mikubwa ya ujenzi inahitaji uwezo mkubwa ambao makandarasi wadogo peke yao uwezo huo hawana na taabu kujenga nguvu hiyo. Lakini, makandarasi wadogo wakiunganisha nguvu zao watakazochangia zitawezesha kujenga uwezo wa kumudu kutekeleza miradi mikubwa. Natoa wito maalum kwa makandarasi wazalendo ambao wengi wao, taarifa inasema ni asilimia 85, ni wadogo kuupa uzito unaostahili wito wangu huu. Naamini mkifanya hivyo kilio chenu kwamba hampewi miradi mikubwa ya ujenzi kitakwisha. Naelewa hisia za wanaogawa kazi kwamba wanatazama uwezo wa makandarasi kwa kila kazi wanayotoa. Kwa vile makandarasi wazalendo walio wengi ni wadogo hawapewi miradi mikubwa. Ndiyo maana nasisitiza kuungana kwenu ili mjenge sifa za kupewa miradi mikubwa.
Aidha, nawaomba mtumie fursa ya financial leasing kupata vifaa. Sherie ile imekusudiwa kuwawezesha watu kupata mitambo ya kufanyia shughuli. Naambiwa benki bado hazijatoa ushirikiano wa kutosha. Nitumie nafasi hii kuziomba benki kutoa ushirikiano unaostahili.

Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanaotoa kazi kuwathamini na kuwaamini makandarasi wazalendo walio wakubwa na wadogo. Mimi naambiwa hata wale wakubwa wanapata taabu kupewa kazi. Wapeni kazi ili na wao wajenge uwezo. Hakikisheni mnaweka wahandisi washauri mahiri ili wasimamie vizuri kazi na kuhakikisha kiwango cha ubora kinachostahili kinafikiwa. Tusipojenga moyo wa kuwaamini na kuwapa kazi kamwe hawatakua na kuwa wakubwa. Watabakia kuwa wadogo milele. Hali hiyo haina maslahi kwa taifa. Tunapenda na makampuni ya Kitanzania nayo yaweze kutoka nje ya mipaka yetu na kuleta sifa na manufaa kwa taifa kama yafanyavyo makampuni ya nchi nyingine. Hatutafika hapo kama hatutachukua hatua za makusudi za kulea na kujenga makampuni ya wazalendo wetu. Si mengi lakini tukijisaidia mawili matatu hayatakosekana.

Ndugu Mwenyekiti;
Jambo la pili ambalo ningependa kulisisitiza leo ni matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya ujenzi.
Ndugu Washiriki;

Sote tunatambua kwamba dunia sasa inapita katika kipindi cha mabadiliko makubwa na ya haraka ya kiufundi na kiteknolojia. Ingawa teknolojia inayozungumziwa sana ni ile ya habari na mawasiliano, ukweli ni kwamba mabadiliko haya yapo katika nyanja zote pamoja na hii yenu ya ujenzi. Mabadiliko haya ya teknolojia ya ujenzi yana athari za namna mbalimbali kwa upande wa ufundi, ubora, ufanisi wa kazi pamoja na gharama. Ni dhahiri kabisa kwamba ujenzi wa majengo au uwekaji lami wa leo na hata muonekano wa barabara ya lami au za udongo ni tofauti sana na ule wa miaka ya 1980. Hivyo basi, rai yangu kwa makandarasi wote ni kwenda na wakati. Watumie ujuzi, maarifa na teknolojia za kisasa katika kazi zenu mzifanyazo. Msibaki nyuma kwa kutumia mbinu na maarifa ya miaka ya nyuma. Hamtaweza kumudu ushindani ambao ndiyo msingi mkuu wa kufanya kazi katika dunia ya leo na ndiyo matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Kukosa ufanisi na ubora kunaongeza gharama, hivyo kuwafanya washindwe kupata kazi. Mwenyekiti amezungumzia suala la kutumia makandarasi kwa majengo ya jamii. Sina tatizo nalo. Nami nalipenda, lakini mmejiuliza kwa nini wananchi wanaona bora watumie fundi mwashi wao badala ya mkandarasi?

Ndugu Mwenyekiti;
Suala la tatu ambalo ningependa kuliongelea ni suala la rushwa katika mchakato mzima wa utafutaji, upatikanaji na utekelezwaji wa miradi (zabuni) katika sekta ya ujenzi.
Mdudu rushwa yupo hata katika sekta ya ujenzi pia. Sekta hii inatumia pesa nyingi na vishawishi vya kutafuta njia za mkato kwa waombaji na watoaji kazi ni vikubwa. Na hivyo kuwa kichocheo kimoja kikubwa cha rushwa. Penye rushwa kazi zimekuwa zikitolewa pasipo kuzingatia matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Makandarasi wasio na uwezo hupewa kazi au usimamizi wa kazi kuwa mbaya. Matokeo yake ni kazi kutokuwa na ubora wala uimara unaostahili. Wakati mwingine kazi huchelewa kukamilika na kusababisha watu kuchelewa au hata kukosa huduma hiyo na kuzua manung’uniko ya wananchi kwa Serikali yao. Wakati mwingine usalama wa watu na mali zao huwa hatarini na kuwatia hasara kubwa wenye miradi (Serikali au watu binafsi) na hivyo kupunguza kasi ya maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Bodi yenu, pamoja na Bodi zingine kama vile Bodi ya Usajili wa Wahandisi, inao pia wajibu mkubwa wa kudhibiti tatizo hili. Ni kwa heshima yenu na manufaa kwa taifa.

Ndugu Mwenyekiti;
Nimefurahi kwamba katika mkutano wenu mtajadili pia athari za mtikisiko wa uchumi wa dunia kwa sekta ya ujenzi. Uchumi wa dunia unapita katika kipindi kigumu. Tatizo limeanzia nchini Marekani na Ulaya, lakini sote tumeathirika. Kuelewa vizuri ukweli kuhusu mgogoro wa uchumi duniani na athari zake kwa uchumi wetu na shughuli za kila mmoja wetu ni jambo muhimu sana kwetu sote. Inatusaidia kujipanga vizuri kukabiliana na athari zake ikiwa ni pamoja na kujihami na kutumia fursa zake.
Mheshimiwa Waziri, Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Washiriki;

Kabla sijamaliza, napenda kuwapongeza wale wote waliopata tuzo za mwaka huu. Tunawapongeza kwa ufanisi wao. Naomba iwe changamoto kwa wengine wafanye vizuri mwakani. Mwisho kabisa, pamoja na yote niliyoyasema, naomba nimalizie kwa kuwaachia changamoto chache, ambazo nina uhakika mnaziweza:
1. Makandarasi wote ni muhimu wafanye kazi kwa kuzingatia usalama wa watu, kuweka mbele ubora wa kazi zao, na kuzingatia muda na gharama iliyopangwa.

2. Makandarasi wote ni lazima wafanye kazi kwa kuzingatia utunzaji na uendelezaji mazingira.

3. Makandarasi wote wahakikishe wanafanya kazi zao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria husika za nchi.

4. Makandarasi wote wawe ni chanzo na chachu ya utoaji na uboreshaji ajira kwa wananchi wa eneo husika la mradi na kwa Watanzania kwa ujumla.

5. Makandarasi wote wawe wepesi na mfano katika kuchangia shughuli za hisani (Corporate Social Responsibility) kama mchango wao na utambuzi wa jamii ambapo miradi yao ipo.

Ndugu Mwenyekiti, Ndugu Washiriki, Mabibi na Mabwana;
Baada ya kusema maneno haya mengi, sasa natamka kwamba Mkutano wa Mashauiriano kwa mwaka 2009 umefunguliwa rasmi. Nawatakia mkutano wenye mafanikio mema. Nasubiri kwa hamu matokeo yake.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Ministry of Infrastructure Development

Tancot House, Pamba Road / Sokoine Drive, P.O. Box 9144, Dar es Salaam | Phone +255 22213 7650 - 6 | Fax +255 222112751