
Hon Dr.Shukuru Kawambwa(MP) Minister of Infrastructure Development


Site Search
Reports & Policies
To facilitate provision of an economic, safe and reliable constriction industry, transport and services, meteorology, government buildings...

Ministry of Infrastructure Development
Its mission is to facilitate provision of an economic, safe and reliable construction industry, transport and services, meteorology, electrical and mechanical services, government buildings and stores that meet the needs of the public through development and implementation of appropriate sector policies, strategies and standards.
Speeches and StatementsHOTUBA YA RAIS, UZINDUZI RASMI WA UJENZI WA BARABARA YA SINGIDA – BABATI – MINJINGUMnamo tarehe 04 Agosti 2009, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua rasmi ujenzi wa barabara ya Singida - Babati - Minjingu.
IFUATAYO NI HOTUBA YA RAIS: Nawashukuruni sana kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika sherehe hii ya kuzindua ujenzi wa barabara ya Singida – Babati hadi Minjingu. Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ningependa kumkaribisha rasmi Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Sipho Moyo. Tunakushukuru sana kwa kuitikia mwaliko wetu kuja kujumuika nasi katika hafla hii. Dkt Moyo karibu sana. Ndugu Wananchi, Kama alivyotangulia kusema Waziri wa Miundombinu, barabara hii ina umuhimu mkubwa kwa nchi yetu na majirani zetu pia. Majirani zetu wa Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na hata Uganda watapata njia mbadala ya kusafirishia mizigo yao kutoka bandari ya Tanga. Bandari ya Tanga ikitumika ipasavyo,itasaidia sana kupunguza msongamano wa meli na makontena katika bandari ya Dar es Salaam. Haya yatawezekana tu pale tutakapokuwa na barabara nzuri na imara. Tukiwa na barabara nzuri tutakuwa na fursa nzuri ya kufanya biashara na majirani zetu hawa. Barabara nzuri ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo kwa kipindi kirefu itaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wetu. Tukiwa na barabara nzuri ni wazi kuwa Wananchi wetu watapata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu. Kwa upande mwingine, mazao yao yatafika sokoni kwa wakati na hivyo wakulima watapata bei nzuri kwa mazao yao. Barabara nzuri ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa maeneo ya mijini na vijjijini. Ni ukweli ulio dhahiri kuwa tukiwa na barabara imara, shughuli za utalii zitaongezeka na huduma za afya, elimu na utawala zitaimarika pia. Ndugu Wananchi, Kwa kuzingatia ukweli huu, Serikali inaendelea kutenga fedha katika bajeti yake na kufanya mazungumzo na Wahisani mbalimbali ili kupata fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Ndugu Wananchi, Tumearifiwa na Katibu Mkuu kuwa ujenzi wa barabara hii utagharimu shilingi bilioni 210. Hizi si fedha kidogo. Kwa miaka mingi Benki ya Maendeleo ya Afrika imekuwa ikitoa misaada kugharamia ujenzi wa barabara zetu kwa nia ya kuimarisha ukuaji wa uchumi wetu, kuondoa umaskini na kuboresha hali ya maisha ya watu wetu. Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania kupitia kwa Mwakilishi wa Benki kuishukuru kwa dhati kabisa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa misaada ambayo imekuwa ikiitoa kwa nchi yetu. ADB ni mshirika wa kweli wa maendeleo ya nchi yetu. Ndugu Wananchi, Mbali ya kuchangia kukuza uzalishaji wa mazao ya kilimo, njia imara za usafishaji zinasaidia kufungua fursa mpya za uwekezaji katika maeneo mengine ya uchumi. Miradi ya ujenzi wa barabara huko vijijini imekuwa ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato kwa wananchi wetu hali ambayo inasaidia kupunguza wimbi la vijana ambao ndio nguvu kazi kukimbilia mijini. Pamoja na juhudi zinazoelekezwa katika ujenzi wa barabara kuu, wakati umefika kuongeza juhudi katika ujenzi wa barabara za mikoa na wilaya ili kuchochea maendeleo vijijini. Ndugu Wananchi, Kwa bahati mbaya uboreshaji wa barabara zetu unaonekana kuambatana na ongezeko la ajali za barabarani. Takwimu zinaonyesha kuwa mikoa yenye barabara nzuri za lami ndiyo inayoongoza kwa kuwa na viwango vikubwa vya ajali za barabarani. Taarifa zinaonyesha kuwa ajali nyingi zinachangiwa na mwendo kasi, ulevi wa madereva, uzembe wa madereva kutozingatia sheria za barabarani na wizi wa alama za barabarani ambazo hutoa tahadhari kwa madereva. Ni hivi majuzi tu wananchi ishirini na nane walipoteza maisha katika ajali mbaya nay a kutisha iliyotokea wilayani Korogwe mkoani Tanga. Serikali haitavumilia kuona hali hii ikiendelea. Wizara ya Mambo ya Ndani iwachukulie hatua kali madereva wote watakaobainika kusababisha ajali kwa sababu za uzembe unaotokana na mwendo kasi, ulevi ama kutozingatia sheria za barabara. Aidha, viongozi wa mikoa, wilaya na vijiji zinapopita barabara za lami wahakikishe kuwa wote wanaohujumu miundombinu ya barabara kwa kuiba alama za barabara wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Endapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake, kwa nafasi yake, nina imani tunaweza kukomesha kabisa ajali ambazo zinaweza kuepukwa. Ndugu Wananchi, Bado tunalo tatizo sugu kwa baadhi ya madereva na wamiliki wa magari ya kusafirisha mizigo na abiria kuzidisha uzito wa mizigo katika magari yao. Tabia hii inachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu barabara zetu. Barabara ambayo kwa kawaida ingedumu kwa miaka 15, inaharibika na kuhitaji matengenezo makubwa baada ya takriban miaka minane tu. Ni muhimu kwa Wizara ya Miundombinu kwa kushirikiana na Wakala wa barabara, (TANROADS) kuhakikisha kuwa zoezi la upimaji na uthibiti uzito wa magari linaendeshwa kwa umakini mkubwa. Endapo mizani iliyopo itatumiwa kwa lengo lililokusudiwa, nina imani barabara zitalindwa kutokana na uzidishaji wa uzito wa magarizetu na hivyo kupunguza gharama za matengenezo na ukarabati wa barabara. Ndugu wananchi, Uzoefu umeonyesha kuwa ujenzi wa barabara za lami unaongeza na kurahisisha mawasiliano kati ya sehemu moja hadi nyingine na hivyo kuongeza shughuli za kijamii na kiuchumi. Kwa bahati mbaya, hali hii inaonekana kuchangia sana ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Sasa hivi kuna ongezeko kubwa la watu kutoka maeneo mbalimbali wanaofuata ajira katika mradi huu. Napenda kutoa wito kwa Wananchi wote kuzingatia ushauri na maelekezo yanayotolewa na wataalamu kuhusu njia sahihi za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu hatari. Kuna umuhimu wa kujiepusha na vitendo au mazingira hatarishi yanayoweza kuchangia maambukizi ya ugonjwa huu ambao hadi sasa haujapata kinga wala tiba. Ndugu wananchi, Naomba nimalize hotuba yangu kwa kuwashukuru tena wenzetu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kukubali kwao kutuunga mkono katika maeneo mengi ya maendeleo hususan uimarishaji wa Miundombinu ya usafiri nchini. Aidha nawashukuru sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia tukio hili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Waheshimiwa Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA. |
More Speeches and Statements
- HOTUBA YA RAIS: MKUTANO WA MASHAURIANO KWA MWAKA 2009 WA BODI YA USAJILI WA MAKANDARASI (CRB)
- HOTUBA YA RAIS: UZINDUZI WA KIVUKO CHA MV. MAGOGONI
- HOTUBA YA RAIS, UZINDUZI RASMI WA UJENZI WA BARABARA YA SINGIDA – BABATI – MINJINGU
- The Global Aviation Safety Roadmap Workshop
- Opening of the International Expert Review Meeting on Regional Climate Outlook Forums
- Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Katika Uzinduzi Rasmi Wa Ujenzi Wa Barabara Ya Mbeya - Lwanjilo
- Speech by the Minister on Challenges and Opportunities for Private Sector Participation
- Speech by the Minister at the High Level Meeting on Almaty Programme of Action
- Speech by the Minister on Multinational Tanzania-Rwanda-Burundi Railway Project
- Opening Speech by the Minister for Infrastructure Development, on Construction Industry Forum
